Ujumbe wa wafanyabishara kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na viongozi wa Mashirika ya Umma Tanzania walifanya ziara nchini Brazil iliyofanyika tarehe 28 Juni hadi 7 Julai, 2019, iliyokuwa na lengo la kutafuta fursa  za kibiashara, uwekezaji na masoko  kwa bidhaa zinozalishwa Tanzania.

Ujumbe huo ulitembelea mji wa Rio de Janeiro mnamo tarehe 28 Juni hadi 2 Julai,2019 na kufanikiwa kuonana kwa mazungumzo na Taasisi mbalimbali za Brazil zikiwemo  Shirika la Umma la Uchimbaji na Utafutaji wa Mafuta  na Gesi la Brazil (Petrobras), Kampuni ya Udhibiti wa Viwango na Uendelezaji  wa Masoko ya Mafuta na Gesi (IBP). Mjini Brasilia kuanzia tarehe 2 hadi 5 Julai, 2019 ambapo walikutana na uongozi wa Wakala wa uwekezaji na Biashara  ya Brazil (APEX), Muungano wa Jumuiya ya Wenye viwanda ya Brazil (NCI) na Taasisi ya Uendelezaji wa Wazalishaji wadogo na Kati (SEBRAE).  

Taasisi nyingine ambazo ujumbe huu ulikutana nazo mjini Brasilia kwa mazungumzo ya ushirikiano ni Bodi ya Utalii ya Brazil (Embratur) na Wizara ya Kilimo hususan idara ya udhibiti wa biashara za Mazao ya Matunda na Mifungo. Mjini Sao Paulo, ujumbe ulionana na Muungano wa Wenye viwanda wa São Paulo (FIESP) na Taasisi ya uendelezaji wa Teknolojia na ubunifu (Agro-Industrial Innovation Incubator-INOVA) na  Jumuiya ya Watanzania (Diaspora)  waishio mjini São Paulo.