Ubalozi ulishiriki katika maonesho wa ng’ombe wa kisasa ya 84 ya Expo-Zebu yalifanyika mjini Uberaba, Minas Gerais kuanzia tarehe 28 Aprili hadi 6 Mei, 2018. Maonesho haya makubwa ya ng´ombe duniani yalifunguliwa rasmi na Rais wa Brazil Mhe. Michel Temer na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa, kidiplomasia, wafugaji wakubwa kwa wadogo pamoja na makampuni zaidi ya hamsini yanayojihusisha na teknolojia za uzalishaji, bidhaa za ufugaji na mazao yake, kama vile ABS, Brazilian Cattle, MATSUDA, Indu-Brazil, Geneal, Biomatrx n.k.

Ujumbe wa Tanzania katika Maonyesho haya uliongozwa na Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi aliyeambatana na Ndugu Iddy Athumani, Mwakilishi wa Wizara ya Mifugo nan a Uvuvi kutoka NARCO-Tanzania. Ushiriki wa Tanzania katika maonyesho haya yalikuwa na lengo la kujifunza namna wafugaji wa Brazil hasa mji wa Uberaba wamefanikiwa katika ubora na teknolojia ya ufugaji wa ng´ombe wa nyama na maziwa, hasa ukizingatia mafanikio makubwa waliyofikia duniani katika uzalishaji wa nyama. Vilevile kupata uzoefu wa uhimilishaji (AI) na “Embryo transfer” kutoka kwenye kituo kikubwa cha ABS pamoja na kupata fursa ya kukutana na wafugaji wakubwa wa ng´ombe wenye mafanikio makubwa katika sekta hiyo.