Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (katikati) akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil, Mhe. Balozi Fernando Jose Marroni de Abreu (hayupo pichani) walipokutana kwa Majadiliano ya Kisiasa yaliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili, 2018. Majadiliano hayo yalifanyika wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili ya Mhe. Balozi Fernando hapa nchini. Pamoja na mambo mengine walijadiliana kuhusu namna ya kuboresha mashirikiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili hususan katika eneo la biashara na uwekezaji.
Pia Naibu Mawaziri hao walijadili namna ya kutekeleza kikamilifu Mradi wa Pamba kwenye eneo la Ziwa Victoria na matokeo ya kusainiwa kwa mkataba wa msamaha wa deni la Tanzania kwa Brazil pia lilijadiliwa. Aidha, Brazil wameahidi kushirikiana na Tanzania kwenye sekta ya afya hususan katika kupambana na maradhi ya Selimundu (Sircle-cell) na kwa upande wa Zanzibar watashirikiana katika afya ya mama na mtoto hususan kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga.

Mhe. Dkt. Kolimba na Ujumbe wake wakifuatilia mazungumzo hayo
Mhe. Fernando de Abreu na Ujumbe wake wakifuatilia mazungumzo
Hati ikisainiwa. Pembeni ya Balozi Nchimbi ni Bw. Mustafa M. Ussi, Afisa Mambo ya Nje kutoka Kitengo cha Sheria .
Mhe. Balozi Nchimbi na Mhe. Balozi Puente wakibadilishana Hati hiyo mara baada ya kusaini huku Naibu Mawaziri wakishuhudia 
Mhe. Dkt. Susan akiwa na Mhe. Balozi Fernando mara baada ya kukamilisha majadiliano 
Picha ya pamoja kati ya Naibu Mawaziri na wajumbe wote wa Tanzania na Brazil 
